JANUARI 1, 2013
MAREKANI
Mashahidi wa Yehova Wauza jengo lao lililokuwa Zamani Hoteli ya Bossert
BROOKLYN, N.Y—Mashahidi wa Yehova wamemuuzia David Bistricer wa kampuni ya Clipper Equity na Chetrit Group, jengo lao lililokuwa zamani Hoteli ya Bossert, lililo katika Mtaa 98 Montague, karibu na jengo la kihistoria la Brooklyn Heights. Bossert ilijengwa katika mwaka wa 1909, mwaka ambao Mashahidi wa Yehova walihamia katika makao yao makuu, Brooklyn Heights.
Mashahidi walianza kutumia jengo hilo katika mwaka wa 1983 na kulinunua mwaka wa 1988. Mara moja walianza kufanya marekebisho makubwa ya jengo lote kulingana na viwango vya Kamati ya Uhifadhi wa Majengo ya Kihistoria vya wilaya (Landmarks Preservation Commission), wakishinda tuzo kwa sababu ya kazi waliyofanya ya kulirudisha jengo hilo katika umaridadi na mvuto uliokuwa nao mwanzoni.
Hivi karibuni, Mashahidi wa Yehova wamepunguza baadhi ya kazi zinazofanywa huko Brooklyn. Kupungua kwa idadi ya wafanyakazi kumepunguza pia uhitaji wa vyumba huko Brooklyn, kwa hiyo jengo hilo likauzwa.
David Semonian, msemaji wa Mashahidi wa Yehova kwa vyombo vya habari anasema hivi: “Kwa miaka 25 iliyopita tulifurahia kulitunza jengo la Bossert. Ni jengo zuri sana nasi tunathamini sana sehemu iliyotimiza katika historia yetu.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
David Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, simu +1 718 560 5000