JANUARI 30, 2017
KOLOMBIA
Mashahidi Nchini Kolombia Wapewa Tuzo na Shirika la Kutafsiri la Lugha ya Ishara
BOGOTA, Kolombia—Shirika la Kitaifa la Watafsiri, Wakalimani, Waelekezi-Wakalimani wa Lugha ya Ishara nchini Kolombia, ANISCOL, pamoja na mashirika mengine mawili ya eneo hilo, yaliwapa Mashahidi wa Yehova tuzo kwa sababu ya vifaa vyao vya lugha ya ishara wakati wa kongamano la kitaifa lililofanywa Oktoba 7-9, 2016. Hilo ndilo kongamano la kwanza lililofanywa kwa ajili ya wakalimani na waelekezi-wakalimani wa lugha ya ishara nchini Kolombia, ambao huwasaidia viziwi na vipofu.
Mashahidi walikaribishwa kwenye kongamano hilo ili wapokee tuzo la kutambua “kazi yao nzuri sana ya kuandaa habari za kidini na jinsi ambavyo wameboresha maisha ya viziwi nchini Kolombia.” Ricardo Valencia López, mmoja kati ya wale waliopanga tukio hilo na ambaye pia ni rais wa Shirika la Wakalimani, Waelekezi-Wakalimani, na Watafsiri wa Lugha ya Ishara ya Kolombia ASINTEC, lililoko katika eneo la Majiji Matatu ya Kahawa, anaeleza zaidi kwamba Mashahidi wa Yehova walikaribishwa kwa sababu “wamechangia kusitawi kwa kazi hiyo kwa kutokeza habari zilizotayarishwa vizuri, ambazo zinatumiwa watu wanapotafuta vigezo vya kazi ya kutafsiri.”
Wakati wa kongamano hilo, Mashahidi walitoa onyesho linalofafanua mambo ambayo wamejionea wakiwa kikundi cha utafsiri na ukalimani. Mambo waliyosimulia yalipokewa vizuri sana hivi kwamba halmashauri iliyopanga kongamano hilo iliwapa Mashahidi tuzo la ziada la kushukuru kwa jinsi onyesho hilo lilivyochochea upendezi wa watu na kuwafanya watoe maelezo mazuri sana.
Cristian David Valencia, mchoraji na mtaalamu wa kutokeza rekodi za video na sauti kutoka eneo la Pereira ambaye alihudhuria kongamano hilo, alisema kwamba “[alishangaa] kuona kwamba jamii fulani ya kidini ina mfumo wa kuelimisha watu wenye mpangilio mzuri sana,” hasa ikizingatiwa kwamba Mashahidi hawalipwi kwa kazi yao.
Wilson Torres, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Kolombia, anasema hivi: “Tumekuwa tukiandaa habari kwa ajili ya viziwi katika eneo hili tangu mwaka wa 2000. Kwenye tovuti yetu, sasa tuna zaidi ya video 400 zilizotayarishwa kwa ajili ya watu wazima, vijana, na watoto wanaotumia Lugha ya Ishara ya Kolombia. Tunaendelea kuandaa habari zinazotegemea Biblia bila malipo, kama tu ilivyo na machapisho yote tunayotokeza.”
Ulimwenguni pote vikundi vya kutafsiri vya Mashahidi wa Yehova vinatokeza na kusambaza video nyingi sana katika lugha 88 za ishara. Mashahidi wa Yehova wametokeza pia programu ya JW Library Sign Language inayowawezesha kupakua, kupanga, na kucheza video za lugha ya ishara kwa urahisi kutoka kwenye tovuti yao rasmi ya jw.org.
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, +1-845-524-3000
Kolombia: Wilson Torres, +57-1-8911530